
Nchini
Tanzania kilimo kimeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa watu wengi kwani
asilimia kubwa ya wakazi hujishughulisha na shughuli za kilimo. Lakini upatikanaji
wa mbolea zisizo na kemikali imeendelea kuwa changamoto na hata zile zilizopo
kutokidhi mahitaji ya soko hivyo kutegemea uagizwaji wa mbolea hizo nje ya nchi
ambazo hufubaisha mnyororo wa uongezaji thamani na kupelekea kupanda kwa bei ya
bidhaa zifikapo sokoni.
Kwa
kutambua umuhimu wa kilimo kwa uchumi wa Taifa, Serikali kupitia Shirika lake lenye
jukumu la kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo nchini, Shirika la Taifa la Maendeleo
(NDC), imeona haja ya kukiongezea uwezo kiwanda chake, Tanzania Biotech Products
Limited (TBPL) cha Kibaha-Pwani kuzalisha mbolea zisizo na kemikali ambazo
zitasaidai kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mbolea zenye ubora na zisizo
na madhara kwa watumiaji.
Leo, Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Naibu Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kighahe wameshuhudia Hafla ya Utiaji Sahini Mkataba wa Uzalishaji Mbolea na Viuatilifu Hai vya kuangamiza wadudu dhurifu katika mazao hasa pamba na mboga katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibaiolojia, Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) cha Kibaha mkoani Pwani kilicho chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Hafla
hiyo iliyofanyika kiwandani hapo imehudhuriwa na ujumbe kutoka Serikali ya Cuba
ambao ni wadau katika uzalishaji wa bidhaa za kibaiolojia, Timu ya Majadiliano
ya Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI
anayeshughulikia Afya, Dkt. Grace Magembe, wafanyakazi wa NDC na TBPL.
Akizungumza
katika hafla hiyo Balozi Mulamula amesema; amefarijika kuona ushirikiano na
uhusiano baina ya Tanzania na Cuba ukiendelea kukua na kukuza diplomasia inayojikita
katika biashara na uwekezaji.
Pia ameeleza
kuwa Serikali imeshuhudia utiaji sahini wa mikataba miwili. Mosi, wa uendeshaji
wa kiwanda pamoja na mkataba wa kuangalia namna teknolojia iliyoletwa na Cuba
itasaidai kuzalisha viuatilifu vitakavyotumika kuzalisha mbolea zisizo na
kemikali pamoja na dawa za kibaiolojia za kuangamiza wadudu dhurifu.
Ikumbukwe
kuwa lengo la ujenzi wa kiwanda hiki lilikua kutokomeza malaria nchini na
Afrika kwa ujumla. Kauli hii inaungwa mkono na Naibu Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji,
Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kighahe ambaye amesema
“Viuatilifu
hivi ni vya kibaiolojia, havina madhara hasi kwa watumiaji,” amesema Mhe.
Kighahe.
Amekazia
kuwa uzalishaji wa mbolea zisizo na kemikali itasaidia kukuza Sekta ya kilimo
kwa kuzalisha mazao yasiyo na kemikali hivyo kulinda afya za watumiaji.
Nae
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge amesema kuwa uwepo wa kiwanda
hicho katika mkoa wake kinawasaida vijana wa Kitanzania kuongeza ujuzi wao
kutokana na teknolojia mpya inayoletwa na Wacuba, licha ya hilo ameeleza kuwa kilimo
cha kutumia mbolea zisizo na kemikali kina soko kubwa.
“Kilimo
hai kina soko kubwa duniani na tukipata bidhaa hizi nchini tutauza kwa bei ya
chini,” amesema Mhe. Kunenge.
Uzalishaji
wa mbolea za kibaiolojia utasaidai kuinua kilimo cha Tanzania na kukifanya kuwa
cha kisasa zaidi, kama alivyoeleza Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa
la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe.
“Hizi ni mbolea za kibaiolojia zinazo zalishwa na bakteria
wanaotoka kwenye udongo na ni bakteria rafiki,” ameeleza Dkt. Shombe. Licha ya
hilo amekazia kuwa uhitaji wa soko ni mkubwa na wanatarajia uhitaji kuongezeka
kwani watu wengi wamekua wakitumia bidhaa zinazo zalishwa na mbolea za
kibaiolojia.